Sunday, November 10, 2013

DIRISHA DOGO KUFUNGULIWA NOVEMBA 15

Usajili wa wachezaji kwa dirisha dogo kwa msimu wa 2013/2014 Tanzania Bara unafunguliwa Novemba 15 mwaka huu na utafungwa rasmi Desemba 15 mwaka huu. Kwa mujibu wa kanuni, klabu zenye fursa ya kusajili wachezaji katika dirisha dogo ni zile ambazo hazijatumia nafasi zote 30 za wachezaji.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zimemaliza duru la kwanza msimu huu. Duru za pili litaanza kutimua vumbi Januari mwakani.
Kwa mujibu wa Kalenda ya Matukio ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) matukio ya Novemba na Desemba ni dirisha dogo la usajili na mechi za kirafiki za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)- FIFA Date.
Matukio mengine ni michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za VPL na michuano ya Kombe la Chalenji itakayofanyika Nairobi, Kenya.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

WANACHAMA MFUKO WA BIMA YA AFYA TANGA WAENDELEA KUONGEZEKA

Na Oscar Assenga,Tanga.
IMEELEZWA kuwa idadi ya wanachama wa Mfuko wa Bima ya Afya mkoa wa Tanga(NHIF) katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita imekuwa ikiongezeka toka 17,487 mwaka 2011-2012 hadi kufikia 17,490 mwaka 2013-2014.
Haya yalielezwa na Mkurugenzi wa uhai na takwimu wa  mfuko wa bima ya Afya nchini (NHIF)Michael Mhando wakati akitoa takwimu hizo katika mkutano wa wadau wa NHIF na CHF mkoa wa Tanga uliofanyika katika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Tanga ambao ulifunguliwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Benedict Ole Kuyani.
Alisema katika kipindi hicho idadi ya wanachama wa CHF imeongezeka kutoka 30,920 hadi 39,932 ambapo ongezeko hilo linadhihirisha kuwa wananchi wamekuwa na hamasa kubwa ya kujiunga na mfuko huo kutokana na kuimarika kwa huduma zake.
Aidha alieleza kuwa kwa kadiri siku zinavyozidi kusogea mbele wananchi wengi zaidi watajiunga na kunufaika na huduma za matibabu kupitia utaratibu wa kuchangia kabla ya kuugua .
Mhando alisema mikutano hiyo ya wadau ni muhimu kwani inawasaidia kubaini matatizo yaliyokuwa yanawakabili wadau wao na hivyo kuwapa nafasi ya kuweka mikakati ya kukabiliana nayo ili kuhakikisha yanakwisha.
Aliongeza kuwa maoni hayo yanawasaidia kufikia maamuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufungua wigo kwa watanzania wengi ambapo hadi sasa kila mwananchi anayetaka kujiunga na mfuko huo anaweza kufanya hivyo.
Mkurugenzi huyo aliwaomba viongozi wa mikoa katika ngazi mbalimbali wafanye mijadala kuhusu huduma za NHIF na CHF/TIKA kuwa liwe ni ajenda ya kuduma katika vikao vyao vya maamuzi ili matatizo yanayoweza kukabiliwa katika ngazi hizo yasisubiri maamuzi ya ngazi za juu.

NENO LA LEO; SERIKALI, BUNGE, WANAHABARI NA KISA CHA ELIAKIM SIMPASA...!‏

Ndugu zangu, Laiti kama Bunge juzi hapa lingepitisha mapendekezo ya Serikali juu ya vipengele vya sheria ya magazeti ya 1976, basi, nayo ingelikuwa ni habari nyingine ya huzuni kubwa kwa Watanzania. Ni habari ya aibu.
Kwamba miaka 50 baada ya Uhuru, pamoja na kuminyika sana kwa wanahabari, bado kuna watendaji Serikalini wanaofikiria kuwaminya zaidi wanahabari.
Ndio, bado kuna wanaofikiria Wanahabari hawa wenye kufanya kazi kwenye mazingira magumu sana wapewe adhabu kali zaidi wanapofanya makosa wakiwa kazini.
Na wakati mwingine inaonekana, kuwa mahusiano ya Serikali na Wanahabari ni kama ya mzazi na mtoto. Kwamba Serikali ni mzazi, ambaye kila anapoona mtoto amekosea, anachofikiria ni kutafuta bakora ya kumchapa. Na mtoto anapoonekana kulifanya tena kosa, basi, mzazi anafikirikia kuongeza idadi ya bakora. Ni mzazi anayetaka kutuhumu na kuhukumu hapo hapo. Ni viboko tu. Hataki na haioni haja ya mtu mwingine aingilie kati kuwasikiliza mzazi na mtoto kwenye kutofautiana kwao.
Na imeripotiwa kwenye Mwananchi, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema juzi ameangukia pua baada ya Bunge kukataa mapendekezo ya Serikali ya kubadili baadhi ya vipengele vya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, ya kuongeza adhabu kwa waandishi wa habari watakaopatikana na hatia ya makosa ya uchochezi.
Mwananchi linaendelea kuandika, kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliungana na wabunge wengine kukataa mapendekezo hayo na kudai kuwa wakati umefika kwa Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria ya vyombo vya habari, badala ya kutoa ahadi zisizo na majibu kila wakati.
Kukataliwa kwa mapendekezo hayo ni pigo kwa Serikali na Jaji Werema ambaye juzi wakati akijibu hoja za wabunge alijigamba kwamba yeye anasimamia amani ya nchi kwa hiyo vifungu hivyo haviwezi kuondolewa, kwani anafanya kazi kwa masilahi ya taifa na hategemei magazeti kwa ajili ya kuwa mbunge. Ni kauli ambayo iliwachefua wabunge. Linaandika gazeti Mwananchi, Ijumaa, Novemba 9, 2013.
Ndugu zangu,
Nahofia, kuwa wakati mwingine wanasiasa wetu wanatunga sheria kwa kuziona 'hatari zilizo mbele yao' zinazotishia maslahi yao binafsi, ya vikundi vyao na ya vyama vyao. Na wala si kwa hatari iliyo mbele yetu kama taifa. Hivyo basi, kauli za kulinda maslahi ya taifa wakati mwingine hutumiwa kama koti la kulivaa kuficha dhamira halisi za hao wenye kuiona ' hatari iliyo mbele yetu'.
Tutafanya makosa kama taifa, kama tutafika mahali hata sheria zetu tutakuwa tukizitunga kutokana na ' hofu' za kisiasa. Hofu za kisiasa ni hisia za kuja na kupita, lakini, yenye kuhusu maslahi ya taifa ni mambo tunayotakiwa kuyajengea msingi na yakabaki hata kama sisi hatutakuwepo duniani.
Majuzi tu hapa alikuja Spika yule wa Bunge la Uswisi na akashangaa kusikia kwenye nchi hii bado kuna magazeti yanafungiwa kwa sheria ya mwaka 1976. Akatwambia kuwa kule kwao anakumbuka mara ya mwisho gazeti kufungiwa ilikuwa ni baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Ndio, Wanahabari wa nchi hii si malaika, nao, kama wanataaluma wengine, wanafanya makosa. Lakini tufike mahali, nasi tufikirie taratibu nyingine za kusahihishana na kupeana adhabu bila kufikiria kwanza adhabu za vifungo vya magerezani. Na kazi ya kusahihishana na kupeana adhabu inaweza kabisa kuachwa kufanywa na wanahabari wenyewe kupitia vyombo vyao husika vya kurekebishana na kuadhibiana. Ndivyo wanavyofanya madaktari, mainjinia, walimu na wengineo. Ikishindikana huko ndiko mahakama zitumike.
Maana, inasikitisha leo kuliona gazeti la Kitanzania likitoka huku likionyesha siku ambazo zimebaki kabla ya gazeti dada kufunguliwa. Maana, kwa maisha ya magazeti ya sasa, hakuna ajuaye amebaki na siku ngapi kabla ya kufungiwa. Mungu tu ndiye ajuaye!
Na katika dunia hii tusiishi tukasahau kanuni za maisha. Kuwa kuna kupanda na kushuka. Kuna leo na kesho. Ya leo unayajua na ya kesho huyajui. Usiyemhitaji leo utamhitaji kesho. Ni kwa vile wewe ni mwanadamu.
Na hapa nitamalizia na kisa cha Mbunge Eliakim Simpasa. Julai 3 mwaka huu, wakati nikitembea kwa miguu Mtaa wa Shaaban Robert jijini Dar, nilikutana na ndugu zangu wawili kwenye familia ya wanahabari; Boniface Makene na John Mapinduzi. Wawili hawa nao walikuwa wakitembea kwa miguu wakiongozana na Mbunge Mstaafu, Mzee Eliakim Simpasa. John na Boniface kwa sasa wako Ofisi ya Makamu wa Rais.
Basi, tukaongea kidogo, na ilibaki kidogo tu nimkumbushe Mzee Simpasa juu ya ugomvi wake na wanahabari, enzi hizo akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki na Maadili.
Maana, nakumbuka siku moja akiwa bungeni, Simpasa alimwomba Spika amwamuru mwandishi wa habari, silikumbuki jina lake, aingie Bungeni na ajieleze mbele ya Bunge juu ya habari potofu aliyoiandika juu ya ' Bunge Tukufu'. Eliakim Simpasa alikuwa kama ' Dikteta' fulani hivi!
Naam, nilisita kumkumbusha Mzee Simpasa, maana, yawezekana mwandishi huyo alikuwa ni John Mapinduzi au Boniface Makene!
Na leo hii ndio hao anaotembea nao mitaani kwa miguu, kama ndugu!
Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa.
Iringa.
0754 678 252
http://mjengwablog.com

JISHINDIE MUDA WA MAONGEZI WA SH 15,000 KWA KUTABIRI MATOKEO YA MECHI YA MAN UTD VS ARSENAL LEO

TOVUTI YA GLOBAL PUBLISHERS LTD, INATOA ZAWADI YA MUDA WA MAONGEZI WA SHILINGI 15,000 KWA MWANACHAMA WAKE YEYOTE ATAKAYETABIRI MATOKEO YA MECHI YA LEO YA LIGI KUU YA ENGLAND KATI YA MANCHESTER UNITED NA ARSENAL FC. ILI KUWEZA KUJISHINDIA MUDA HUO, TUMA MATOKEO YAKO PAMOJA NA NAMBA YAKO YA SIMU KATIKA ENEO LA COMMENTS HAPO CHINI (MFANO: MANCHESTER UNITED 1, ARSENAL 2  0717 121030). ATAKAYEWAHI KUTABIRI NDIYE ATAIBUKA MSHINDI NA ATAPATIWA ZAWADI YAKE KESHO JUMATATU. MWISHO WA KUTABIRI NI SAA 1:00 LEO USIKU. NB: SHINDANO HILI PIA LINAPATIKANA KWA WANACHAMA WETU KWENYE UKURASA WA FACEBOOK WA WWW.FACEBOOK.COM/GLOBALPUBLISHERS KAMA BADO SIYO MWANACHAMA, INGIA SASA NA U-LIKE UKURASA HUO UWEZE KUJISHINDIA MUDA WA MAONGEZI.

Monday, September 2, 2013

HENRY JOSEPH AITWA TAIFA STARS

Mchezaji Henry Joseph wa Simba. Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amemjumuisha mchezaji Henry Joseph wa Simba kwenye kikosi chake kinachojiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul.
Tayari Joseph amesharipoti kwenye kambi ya timu hiyo iliyoko hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam. Taifa Stars ambayo iko chini ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini tangu Agosti 29 mwaka huu, na leo jioni itafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Programu ya timu hiyo inaonesha kuwa kesho (Septemba 3 mwaka huu) itafanya mazoezi yake asubuhi na jioni kwenye uwanja huo huo wa Kumbukumbu ya Karume.
Wakati huo huo, kesho (Septemba 3 mwaka huu) saa 6 kamili mchana Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari.


DAR ES SALAAM FILAMU FESTIVAL KUFANYIKA SEPT 24-26 MWAKA HUU

Tunayofuraha kukupa taarifa rasmi kuwa Tasnia ya Filamu Tanzania sasa imepata tamasha la kuonyesha sinema za kiswahili (Bongomovies).
Tamasha litafanyika tarehe 24-26, Septemba 2013, katika Viwanja Vya Posta-Kijitonyama.
Pia Workshop, Exhibition na Film Forum vitafanyika.
Kiingilio ni Bure!!!!
Samabaza Ujumbe kwa wapenzi wa filamu.
Kwa habari zaidi tembelea www.filamucentral.co.tz 
Na kwa taarifa zaidi sikiliza na tazama vyombo vya habari

GEORGE BUSH ATANGAZA KIFO CHA MANDELA WAKATI HAJAFA

Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush amejikuta ‘akiingia chaka’ kwa kutangaza ‘kifo’ cha Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela ambaye bado yuko hai.
 
Kosa hilo limetokea jana asubuhi (September 1) kwa bahati mbaya baada ya msemaji wa rais huyo wa 41 wa Marekani kujichanganya kwa kutosoma vizuri habari inayomhusu Mandela kupitia Washington Post hivyo kumfanya Bush aandike ujumbe huu,

“Barbara and I mourn the passing of one of the greatest believers in freedom we have had the privilege to know. As President, I watched in wonder as Nelson Mandela had the remarkable capacity to forgive his jailers following 26 years of wrongful imprisonment — setting a powerful example of redemption and grace for us all. 

He was a man of tremendous moral courage, who changed the course of history in his country. Barbara and I had great respect for President Mandela, and send our condolences to his family and countrymen.”
 
Baada ya kosa hilo kutokea msemaji wa Bush, Jim McGrath alitweet kuomba radhi na kukiri kupitiwa na kufanya kosa la kijinga “The 41 stmnt sent this morning was the result of my mis-reading the header on the WaPo news flash. Stupid mistake by me. Apologies to all,”.




Upande wa Afrika Kusini walirekebisha taarifa hiyo kwa kusema Nelson Mandela yuko hai na wanaamini hilo lilikuwa ni kosa tu, hivyo hawatalichukulia kama kitu kikubwa sana. 
“It is clearly incorrect. We see it as an error on his side’ and aren’t going to ‘make a big deal about it”, alisema msemaji wa rais wa Afrika Kusini Mac Maharaj. 
 
Nelson Mandela aliruhusiwa kutoka hospitali jana Jumapili (September 1) baada ya kulazwa tokea (June) akisumbuliwa na matatizo ya mapafu, lakini inasemekana hali yake bado si nzuri sana.
Source: Mail Online