Mtu mmoja raia wa Kenya, Joshua Mulundi (21) jana alasiri alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na makosa ya kumteka na kutaka kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dkt. Ulimboka Stephen.
Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya mbele ya Hakimu Agnes Mchome, alidai kuwa Mulundi ambaye makazi yake Murang'a nchini Kenya, anadaiwa kuwa Juni 26 mwaka huu, akiwa eneo la Leaders Club alimteka Dkt. Ulimboka.
Komanya alidai shitaka la pili ni kuwa Juni 26 mwaka huu, akiwa katika eneo la Msitu wa Mwabepande Tegeta, Dar es Salaam kinyume na sheria mshitakiwa huyo alijaribu kumsababishia kifo Dkt. Ulimboka.
Hakimu Mchome alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo isipokuwa Mahakama Kuu.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Mulundi alidai kuwa kosa aliloshtakiwa nayo siyo sahihi.
Hata hivyo, Hakimu Mchome alimwambia kuwa shauri hilo linasikilizwa Mahakama Kuu na siyo Mahakamani hapo.
Kesi imehairishwa hadi Agosti 5 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa, na mshitakiwa amerejeshwa rumande.
Juni 27 mwaka huu, Dkt.Ulimboka aliokotwa na msamaria mwema katika msitu wa Mwabepande akiwa amejeruhiwa vibaya na kisha akafikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa na maumivu makali na kuanza kutibiwa lakini siku chache baadaye Madaktari waliokuwa wakimtibu walisema wameshindwa kumtibia katika hospitali hiyo kwa sababu hakuna vifaa, hivyo wakamsafirisha kwenye nchini Afrika Kusini ambako hadi sasa anaendelea na matibabu.
No comments:
Post a Comment