Wednesday, August 7, 2013

Tottenham yatoa picha ya Bale kwenye akaunti yao ya Twitter.

Tetesi za kiungo mshambuliaji wa Tottenham Hotspurs kuwa mbioni kujiunga na klabu ya Real Madrid zimezidi kushika kasi baada ya klabu hiyo kushusha picha ya kiungo huyo kwenye ukurasa wao wa mtandao wa kijamii wa twitter.
Ukurasa wa Twitter wa klabu ya Tottenham ulikuwa na picha kubwa za wachezaji Gareth Bale na Clinton Dempsey lakini picha hizo zilitolewa baada ya Dempsey kujiunga na timu ya Seattle Sounders ya Marekani.
Kuondolewa kwa picha ya Bale ndio kumezua gumzo kubwa kwani inaonyesha kuwa tayari Spurs wameanza kuchukua hatua za kusonga mbele na kuanza maisha bila ya nyota huyo ambaye kwa kiasi kikubwa ametokea kuwa alama ya klabu hiyo.
Wiki iliyopita nyota huyo wa kimataifa wa Wales aliwaaga wachezaji wenzie kwenye kikosi cha Spurs   Saa chache kabla ya wachezaji hao kuondoka kwenda nchini Ufaransa ambako walikuwa wanacheza mechi ya Kirafiki dhidi ya Monaco .
Real Madrid na Tottenham zimekuwa kwenye mazungumzo juu ya usajili wa Bale na mazungumzo hayo yamechukua muda mrefu kutokana na msimamo wa klabu hiyo ya London wa kutaka fedha yote huku Madrid wakitaka kulipa kwa awamu .
Pamoja na mazungumzo hayo kuchukua muda mrefu Madrid wanatarajia kumthibitisha Bale kama mchezaji wao siku yoyote kabla ya kumalizika kwa kipindi cha usajili wakati wa majira ya joto.


No comments:

Post a Comment